MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amevunja sekretarieti ya chama hicho inayoongozwa na Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, hatua inayoelezwa kufuatiwa na maamuzi mazito zaidi.
Uamuzi huo wa Kikwete umefanyika usiku huu, huku hali ikiendelea kuwa tete mjini Dodoma kunakofanyika vikao vya chama hicho vilivyotanguliwa na sekretarieti na baadae Kamati Kuu.
Kwa mujibu wa habari hizo, Kikwete toka jana ameonekana kuwa mkali na ambaye amekua akitembea na ajenda mkononi huku wasaidizi wake wengine wakiwa hawaelewi undani wa ajenda yake ya mageuzi mazito ndani ya CCM.
??Moto ulianza kuwashwa katika kikao cha Kamati Kuu ambako zile tetesi kwamba kuna mkakati wa kumuondoa Kikwete zilipodhihiri kuwa kweli ilipoibuka ndani ya Kamati Kuu hoja ya “kutenganisha kofia za Urais na Uenyekiti”
Taarifa ambazo ziliifikia mtandao wa Jamiiforums.com zilieleza kwamba Kikwete alipoona hoja hiyo imetajwa ndipo alipobaini kuwa “sasa mafisadi wamepania kumng’oa”.
Katika kamati kuu hoja ilikua ni nini kifanyike kuwadhibiti watuhumiwa wa ufisadi na pia kuhusu hatima ya Makamba.
Imeelezwa kwamba mjadala wa vikao vya Dodoma utazingatia hotuba ya Kikwete katika sherehe za CCM Februari 5, 2011.
Katika hotuba hiyo Kikwete alisema;
“Hatuwezi kuacha jukumu la kugharamia uendeshaji wa Chama chetu mikononi mwa wafadhili matajiri. Tunahatarisha uhuru wa Chama chetu.
“Chama cha Mapinduzi kiige tabia ya nyoka ya kila baada ya muda fulani hujivua gamba lake na kupata jipya.
“Hatuna budi kufanya hivyo na kufanya hivyo sasa. Wakati wa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa vya tathmini tutalijadili pia suala zima la mageuzi katika Chama.
“Nitapenda tuelewane juu ya namna tutakavyotekeleza agenda hii muhimu kwa uhai na maendeleo ya Chama chetu. Hili ndugu zangu haliepukiki.
“Lazima tukihuishe ili kukiongezea mvuto mbele ya watu. Tuutazame muundo wetu kama unakidhi haja.
“Tuwatazame viongozi watendaji kama wanakidhi haja na kama siyo mzigo unaokipaka matope Chama chetu. Wale tunaoweza kuachana nao sasa tuachane nao kwa maslahi mapana ya Chama chetu.”